Thursday, May 4, 2017

RC -PAUL MAKONDA AONGOZA MAHAFALI YA KIDATO CHA NNE

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka wazazi na walezi kuwaacha huru watoto wao kuendelea na masomo wayapendayo badala ya kuwachagulia. Mwito huo ameutoa katika mahafali ya 32 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Jitegemee JKT Mgulani Dar es Salaam jana ambapo alikuwa mgeni rasmi. “Watoto wapewe uhuru wa kile wanachopenda kukisomea badala ya kuwachagulia kwa kufanya hivyo itawasaidia kupenda kazi watakayoifanya kutokana na masomo waliyosoma” alisema Makonda. Alisema hivi sasa kuna changamoto kubwa kwa watumishi kujiingiza katika vitendo vya ubadhirifu kutokana na kutokuwa wazalendo kutokana na kufanya kazi ambayo imetokana na masomo ambayo hawakuyapenda. Alisema kama mtoto anapenda kuwa mtaalamu wa kompyuta muache aendelee na masomo ya kompyuta badala ya kumlazimisha kuwa na taaluma nyingine. Mkuu wa Shule hiyo, Luteni Kanali Robert Kessy alisema wahitimu hao wameandaliwa vizuri kwa ajili ya kufanya mtihani wao watakao uanza Jumanne wiki ijayo na kuwa wanategemea wote watafanya vizuri. Kessy alisema kuhitimu kidato cha nne ni hatua nyingine ya kuendelea na elimu ya juu hivyo aliwataka wahitimu hao kuondoa wasiwasi katika kipindi hiki cha kuelekea kufanya mtihani wa mwisho. Wakisoma risala yao kwa mgeni rasmi Paul Makonda wanafunzi hao walisema changaoto kubwa waliyonayo na uchakavu wa miundombinu shuleni hapo kama mapaa ya vyumba vya madarasa kuezekwa kwa mabati aina ya Asbestors ambayo si mazuri kiafya pamoja na uchakavu wa sakafu ambapo Makonda aliahidi kutoa mabati 2,000 kwa ajili ya kuezekea vyumba 25. Katika hatua nyingine Makonda amezitaka shule za sekondari za jeshi katika mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha zinaunda kamati kwa ajili ya kurudisha heshima ya michezo mashuleni kama ilivyokuwa awali.

No comments: